Monday, October 29, 2012

Profesa Mukandala awapa somo wahitimu UDSM

Dar es Salaam

WAHITIMU wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), wametakiwa kutumia taaluma zao katika kuikomboa nchi, pamoja na kujikwamua wao wenyewe kiuchumi. Akizungumza mwishoni mwa wiki chuoni hapo, katika mahafali ya 42, Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa Rwekaza Mukandala, alisema elimu waliyoipata wahitimu hao, itumike kuwakwamua wao binafsi pamoja na nchi kwa ujumla, kwani wametumia kodi za wananchi kupata elimu hiyo.

"Sisi kama viongozi tumefurahi kwa hatua hii ambayo mmeifikia leo, lakini tunawashauri, kwamba msibweteke, endeleeni kusonga mbele zaidi na mtumie taaluma yenu kwa maslahi ya jamii na taifa kwa ujumla," alisema Mukandala.

Mukandala alisema, uongozi wa chuo hicho umeandaa dira ya nusu karne ijayo, ambapo ifikapo mwaka 2061, watakuwa wanatoa elimu bora yenye viwango vya kimataifa, kwa kuwa lengo ni kukifanya chuo hicho kiwe kinara wa utoaji elimu ya juu yenye ubora duniani.

"Tutajitahidi kuboresha miundombinu ya elimu ndani ya chuo chetu, ikiwa ni pamoja na kuboresha zaidi ufundishaji wa shahada za awali na kujikita katika kupanua udahili katika shahada za uzamili na uzamivu," alisema.

Aliongeza kwamba, chuo hicho kimejipanga kutumia kikamilifu fursa zilizopo za matumizi ya teknolojia ya mawasiliano ya kompyuta kama mhimili wa shughuli zote za chuo.

Alisema kwamba, mwaka huu jumla ya wahitimu 4,581 walitunukiwa shahada mbalimbali, ambapo wahitimu 2,316 tayari wametunukiwa na wengine 1,363 watatunukiwa shahada zao Novemba 3, mwaka huu.

Mukanda alisema, uwiano wa jinsia kati ya wahitimu wanawake ni asilimia 36, ambayo ni sawa na asilimia 33 kwa wahitimu wa shahada za uzamili na asilimia 37 kwa wahitimu wa shahada za awali.

Pia alisema chuo hicho, kitawatunukia pia shahada 902 wahitimu wa kilichokuwa Chuo Kikuu cha Ardhi na Usanifu wa Majengo (UCLAS) na kwamba, utaratibu huo utafanyika, baada ya kumalizika kwa kesi iliyofunguliwa na UDSM kupitia UCLAS mwaka 2007.

Alisema kwamba, katika hukumu iliyotolewa na Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam Januari 1o mwaka 2011, ilisema walalamikaji wanastahili kupewa vyeti na UDSM, uamuzi ambao ndiyo unatekelezwa.

0 comments:

Copyright © 2012 MeNaco.com Academic News and
Blog created by MeNaco.com